Mvulana Emmanuel Ndiazi wa Shule ya Msingi ya Kitale apokea tuzo baada ya kuibuka mshindi wa uandishi wa Kiswahili kwenye hafla ya kutuza washindi bora mashindano ya eKitabu Digital Essay Competition 2017, Sarit Centre, Westlands, jijini Nairobi Jumatano 27, 2017. Picha/ SAMMY WAWERU
Na SAMMY WAWERU
Imepakiwa - Thursday, September 28 2017 at 06:51
Kwa Mukhtasari
Hafla ya tano ya kuwatuza washindi wa shindano la uandishi wa insha linaloandaliwa kila mwaka na kampuni ya eKitabu na wadhamini wengine mwaka 2017 imewahusisha washiriki wenye mahitaji maalumu, hasa wale wa shule za vipofu nchini Kenya.
HAFLA ya tano ya kuwatuza washindi wa shindano la uandishi wa insha linaloandaliwa kila mwaka na kampuni ya eKitabu na wadhamini wengine mwaka 2017 imewahusisha washiriki wenye mahitaji maalumu, hasa wale wa shule za vipofu nchini Kenya.
Shindano hili lina dhamira ya kunoa vipaji na uandishi wa Insha kwa lugha ya Kiswahili, Kiingereza, Kifaransa na vilevile katika Sanaa.
Washiriki waliofanya vyema walituzwa jana Jumatano sambamba na makala ya 20 ya Kutangaza Vitabu Nairobi yaliyoandaliwa Sarit Centre, Nairobi.
"Shabaha yetu ni kukuza sekta ya elimu kupitia mfumo wa teknolojia ya kisasa, kufadhili shule vitabu kwa njia ya kieletroniki kando na kuchapisha vitabu hivyo kwenye mtandao wetu. Pia tunawajumuisha wanafunzi wa shule ya msingi kuanzia darasa la tano hadi la nane na shule ya upili kwenye mashindano ya uandishi, na kuwatuza wanaoibuka bora," ameeleza Bi Mercy Kirui, Meneja wa Uhasibu na Uchapishaji, eKitabu kwenye hafla ya tuzo ya mashindano ya eKitabu Digital Essay Competition 2017, Sarit Centre Nairobi.
La kutia moyo ni kwamba mashindano hayo yanajumuisha shule za walemavu kutoka dira tofauti za taifa, ambao pia wameibuka kifua mbele kupokea tuzo.
Mada ya mwaka huu imekuwa; “Ni vipi teknolojia inabadilisha shule yako?”
"Kwenye usahihishaji wa uandishi huo tunazingatia ubunifu na jinsi mtahiniwa anapasha ujumbe. Lengo kuu likiwa; 'Nani yuko kwenye mfumo wa digitali?' Ifahamike kwamba dunia inabadilika na kuingia utandawazi wa teknolojia ya kisasa, tunataka kuenda na wakati, hivyo basi watoto wetu wakue na mwendo wa teknolojia kwa sababu itafikia wakati mambo yote yatakuwa yakifanywa kielektroniki," asema Bi Kirui.
Kuna viwango viwili vya majaji wanaopiga msasa uandishi wa wanafunzi. "Jaji wa kwanza ni mwalimu/walimu wa shule zinazoshiriki mashindano hayo kwa kutupa makala ya wanafunzi wao, kisha kuna jopo letu la e-Kitabu kwa ushirikiano na muungano wa Kenya Publishers Association (KPA) tunaosahihisha na kutoa uamuzi wa mwisho kuteua washindi," akaeleza Bi Kirui.
Mashindano ya mwaka huu yameshirikisha shule kutoka kaunti 41 nchini. "Mwaka jana (2016) tulishirikisha kaunti zote 47, kuna shule ambazo mfumo wa teknolojia haujaweza kufanikishwa," akadokeza Bi Kirui.
Kwenye uandishi wa Insha ya Kiingereza kiwango cha shule za msingi tuzo kuu imemwendea mwanafunzi wa shule ya Golden Tott, Kaunti ya Kakamega Purity Ongachi, kwa kuibuka mshindi. Aidha Irene Mbithe wa shule ya upili ya Machakos Girls, Kaunti ya Machakos ndiye ameibuka mwanafunzi bora kwenye uandishi wa Kiingereza.
Owino Agneta wa Shule ya Msingi ya Vipofu ya St Oda, Siaya ndiye amepata tuzo ya uandishi bora wa Kiingereza.
Shule ya Upili ya Vipofu ya Thika imetoa mwanafunzi bora wa uandishi wa Somo hili ambapo Nancy Kinyua ndiye ametuzwa.
Somo teule la Kiswahili uandishi wake shule ya msingi mvulana Emmanuel Ndiazi wa shule ya Kitale Primary, Kaunti ya Trans Nzoia ametawazwa kuwa mshindi bora, huku tuzo sawia na hiyo ya uandishi wa Somo hili shule ya Upili ikipokezwa Linus Lengo wa Malindi High, kutoka Kaunti ya Malindi.
Katika shule za walemavu, zawadi ya Kiswahili imemwendea Vanice Nyaboke wa shule ya msingi ya State Order Primary School for the Blind, iliyoko Kaunti ya Siaya. Tuzo kama hiyo imezawadiwa Pius Muite wa Thika High School for the Blind.
Sekta ya Sanaa pia haijasazwa nyuma, Melody Wambui Njuguna wa Thika Road Primary School ndiye amepokea tuzo hiyo. Okoti Alvin wa Chavakali High School, Vihiga pia ameibuka mshindi kwenye Sanaa.
Shule nyingi hapa nchini zimekumbatia kufunza lugha za Ughaibuni. Kampuni ya e-Kitabu kwa shirikiano na washika dau husika, vile vile imetambua mwanafunzi bora wa lugha ya Kifaransa.
"Katika Lugha ya Kifaransa ni shule tano pekee kote nchini zilizoshiriki, tuzo hiyo imenyakuliwa na Diainah Esther wa Shule ya Kitaifa ya Moi, Eldoret Uasin-Gishu," akadokeza Bi Kirui wakati wa kutambua na kuzawadi waandishi bora.
Walioibuka washindi wametuzwa nakala za vitabu, vitabu vya kielektroniki, tarakilishi, vipakatalishi na zaidi ya hayo kulipiwa karo kima cha Sh50,000 mwaka ujao 2018.
Watahiniwa waliofikwa taji la tuzo walishiriki mashindano hayo kati ya Aprili 20 hadi Julai 20, mwaka huu 2017.
Wakionekana kujawa na furaha na ukwasi wa tabasamu baada ya kutambuliwa kuwa magwiji kwenye masomo hayo, baadhi ya wanafunzi wamepongeza mradi huo. "Kila kitu maishani kinahitaji uvumilivu, na bidii. Ninawashishi wanafunzi wenzangu kote nchini washiriki mashindano haya mwaka ujao. Yanasaidia mtahiniwa kujua mengi na zaidi ya yote kunoa makali ya elimu ikikumbukwa kwamba teknolojia mpya ndio nusu ya kuonana," akasema Diainah Esther, mshindi wa tuzo kategoria ya Lugha ya Kifaransa kutoka Moi Girls High School, Uasin-Gishu kwenye mahojiano ya kipekee na Swahilihub baada ya kuzawadiwa.
"Kwa niaba ya wenzangu ninatoa shukrani za kipekee kwa wafadhili wa mradi huu, kwa kweli unatufaa sisi kama wanafunzi," akaongeza Linus Lengo wa shule ya Malindi High, Kaunti ya Malindi na aliyeshinda tuzo ya mwandishi bora wa Kiswahili.
Mkurugenzi wa eKitabu Bw Will Clurman amesema kuna haja ya wanafunzi, walimu, wazazi na washikadau husika katika sekta ya elimu kuzingatia umuhimu wa mfumo wa teknolojia mpya.
"Tunapania kufanya masomo yawe ya kuvutia na muhimu zaidi kwa watahiniwa. Dunia inabadilika na kuingia kwenye mfumo wa teknolojia ya kisasa, tusiachwe nyuma tuende na wakati ili tukuze elimu," akasema Will.
Licha ya msukosuko wa kisiasa unaoshuhudiwa nchini, Will amedokeza kuwa idadi ya walioshiriki mashindano hayo imeimarika.
"Mwaka huu tumepiga hatua kwa kujumuisha walemavu kwa ushirikiano na idara ya elimu na washikadau husika. Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu, tukitaka kuenda mbali tusafiri pamoja kwenye mtumbwi huu wa elimu," akaeleza.
Kauli ya Afisa huyu imeungwa mkono kwa dhati na Naibu Mkurugenzi wa Taasisi ya Mtaala wa Elimu nchini KICD Bw John Kimotho, aliyewakilisha serikali kwenye mashindano hayo.
"Mfumo huu utawezesha shule zetu kuwa katika utandawazi wa kidijitali. Itakuwa rahisi kwa watahiniwa kupokea mafunzo na kufanya tafiti zao wenyewe," amesema Bw Kimotho.
Ahadi
Aidha ameahidi kwamba serikali itaendelea kushirikiana na eKitabu kuendesha mradi wa elimu kwa wanafunzi kupitia mfumo wa teknolojia ya kisasa. "Tujitie moyo kuendelea kukumbatia mfumo huu. Tushawishi wale ambao hawajafahamu umuhimu wake," akaongeza.
Mwenyekiti wa muungano wa wachapishaji vitabu na makala nchini KPA Bw Lawrence Njagi aidha amepongeza mradi huu akisema ni njia mojawapo ya kuunganisha Wakenya.
"Mada ya mwaka 2017 imekuwa 'Utangamano kupitia vitabu', hii ni njia mojawapo ya kupigana na donda ndugu la ukabila ili tuishi kama jamii moja. Watoto wetu wakikua kwa msingi huu, ukabila tutauzika katika kaburi la sahau," akasema Bw Njagi.
"Sote tukumbatia swala hili. Kupitia usomaji na mafunzo, tutaweza kuzuru maeneo mbali mbali nchini kando na kuhubiri amani," ameongeza akiahidi kwamba KPA itaendelea kushirikiana na eKitabu.
Kulingana na e-Kitabu ni kwamba inalenga kupanua huduma zake kwa kujumuisha masomo kama vile Sayansi, Hisabati, Jiografia na Historia.